Kanuni za Mitihani


Kanuni za Mitihani

1. Watahiniwa wataruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa mtihani angalau dakika 20 kabla ya kuanza kwa mtihani, na hataruhusiwa kuondoka ukumbini mpaka baada ya dakika thelathini kumalizika . Vile vile watahiniwa hawataruhusiwa kuondoka kwenye ukumbi wa mtihani dakika thelathini kabla ya mtihani kumalizika. Hakuna mtahiniwa atakayeruhusiwa kuingia katika ukumbi wa mtihani zaidi ya nusu saa baada ya kuanza kwa mtihani wowote. Mtahiniwa anayeingia katika ukumbi wa mtihani ndani ya nusu saa ya kuanza kwa mtihani ataruhusiwa kuingia katika ukumbi wa mtihani, lakini hataongezwa muda wowote kufidia muda aliyochelewa.

2. Watahiniwa watapewa dakika kumi (10) za kusoma maswali kabla ya kuanza kujibu.

3. Msimamizi Mkuu wa mtihani atatoa matangazo yoyote yanayotakiwa kwa watahiniwa kabla ya kuanza kwa mtihani.

4. Bahasha zenye mitihani zilizofungwa na kutiwa lakiri kwa awamu hiyo zitafunguliwa mbele ya watahiniwa.

5. Mtahiniwa yeyote akitaka kuondoka ukumbi wa mtihani kwa muda sababu yoyote ile, anaweza kufanya hivyo kwa idhini ya MSIMAMIZI MKUU / MSIMAMIZI MWANDAMIZI na atasindikizwa na MSIMAMIZI MSAIDIZI.

6. Kila mtahiniwa atatakiwa kukaa kwenye dawati lenye namba yake ya mtihani.

7. Bodi haitaruhusu visingizio vyovyote kutoka kwa mtahiniwa atakayeshindwa kutoa kitambulisho cha mtihani kinachomruhusu mtahiniwa kuingia kwenye ukumbi wa mtihani,

8. Hakuna mtahiniwa atakayeruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa mtihani bila ya kuwa na kitambulisho cha mtihani alichopewa na barua ya kudahiliwa kwa mtihani.

9. Watahiniwa ni marufuku kuingia kwenye ukumbi wa mtihani, wakibeba au kuwa na aina yoyote ya vitabu na viandikia zaidi ya vile vilivyoruhusiwa na Bodi. Mifuko, mabegi ya mkono na kadhalika ni lazima viachwe mahali palipo bainishwa na msimamizi wa mtihani lakini Bodi haitahusika na upotevu wa vifaa hivyo

10. Simu za mkononi zisiingizwe kwenye ukumbi wa mtihani kwa sababu watahiniwa hawaruhusiwi kupiga simu, kupokea simu, kutuma au kupokea ujumbe wa simu, kutumia nyenzo za simu za mkononi kama vikokotozi au saa wakati mtihani ukiendelea.

11. Mtahiniwa haruhusiwi kuondoa kitabu chake cha kujibia mtihani kutoka ukumbi wa mtihani.

12. Mtihiniwa asijihusishe na mwenendo wowote usiokuwa wa kitaaluma uliokusudiwa kumsaidia katika kufanya mtihani.

13. Katika kila mtihani, watahiniwa watatakiwa watie sahihi kwenye namba zao za mtihani katika karatasi ya mahudhurio.

14. Ni jukumu la kila mtahiniwa kudumisha mazingira ya utulivu katika ukumbi wa mtihani na kuhakikisha kwamba hatashiriki au kuanzisha mazungumzo yoyote au mwenendo utakaoharibu au kuathiri utulivu wa mtahiniwa mwingine yeyote.

15. Kila mtahiniwa anatakiwa kuandika Namba yake ya mtihani kwenye jalada tu. Majina, vifupisho au alama nyingine yoyote itakayomtofautisha mtahiniwa mmoja na mwingine zisiandikwe kwenye jalada la kitabu cha mtihani au karatasi za majibu.

16. Watahiniwa watatakiwa kufuata maelekezo yoyote ya jumla yanayoweza kutolewa na msimamizi Mkuu/ Msimamizi Mwandamizi na kusoma kwa makini maelekezo yaliyoandikwa juu ya karatasi za maswali ya mtihani kama vile yale yanayoonesha idadi ya maswali yanayotakiwa kujibiwa . Zingatia hasa maelekezo yaliyoandikwa kwenye jalada la kitabu cha majibu.

17. Watahiniwa hawaruhusiwi kuvuta sigara, kunywa au kula ndani ya ukumbi wa mtihani.

18. Watahiniwa watataarifiwa juu ya kumalizika kwa mtihani dakika thelathini kabla ya muda wa mtihani kuisha na wakati msimamizi Mkuu/ Msimamizi mwandamizi atakapotangaza kuisha kwa muda wa mtihani, watahiniwa watalazimika kuacha kuandika mara moja. Maelekezo haya yanatumika si kwa kujibu maswali tu, bali pia kwa kujaza hata namba za maswali ,vituo na uandikaji mwingine wowote.

19. Watahiniwa ni lazima wabaki kwenye viti vyao mpaka msimamizi akusanye vitabu vya majibu. Kila mtahiniwa anatakiwa kuhakikisha anakabidhi kitabu chake cha majibu kwa msimamizi.

20. Majibu ya maswali yanatakiwa kuandikwa katika kitabu cha majibu kilichotolewa kwa kadiri ya maelekezo yafuatayo:-

  • Jibu la kila swali lazima lianze kwenye ukurasa mpya.
  • Namba ya swali iandikwe juu ya ukurasa kwenye nafasi iliyotolewa.
  • Andika kwenye pande zote za karatasi ya majibu.
  • Majibu yanatakiwa kuandikwa kwa kalamu ya wino,grafu na michoro lazima ichorwe kwa kalamu penseli
  • Njia zote za kufikia majibu ziandikwe kwenye kitabu cha majibu.
  • Usichomoe au kuchana karatasi yoyote kutoka kwenye kitabu cha majibu. Kata kazi zote zisizohitajika kusahihishwa kwa unadhibu. Usitumie wino wa kufutia maandishi.
  • Iwapo kitabu kikuu cha kuandikia majibu kimejaa unaweza kuomba kitabu cha ziada cha kujibia maswali
  • Weka alama ya tiki (Ö) kwenye maswali yaliyojibiwa ipasavyo.
  • Funga kwa makini vitabu vyovyote vya majibu vya nyongeza na kitabu kikuu cha majibu, na hakikisha kuwa karatasi zote za grafu zimefungwa kwa unadhifu ndani ya kitabu cha majibu na baada ya hapo jaza viboksi kwa usahihi.

21. Majibu yaandikwe kwa unadhifu na kwa mwandiko unaosomeka. Mpangilio wa majibu utazingatiwa wakati wa kusahihisha kila swali. Watahiniwa wanaonywa kwamba majibu yasiyosomeka yatawaathiri katika usahihishaji.

22. Matumizi ya vikokotozi vya kielekroniki visivyo na sauti vinaruhusiwa. Watahiniwa ni lazima walete kalamu zao na wanashauriwa kuleta rula pia.

23. Iwapo kutokana na ugonywa, mtahiniwa atashindwa kuhudhuria mitihani, atamwarifu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi kabla ya kuanza mtihani kwa maandishi. Sehemu ya ada inaweza kurudishwa au inaweza kupelekwa mbele kutokana na hiari ya Kamati ya Elimu na Machapisho. Hakutakuwa na kuomba kurudishiwa ada ya mtihani kwa mtahiniwa anayeahirisha mtihani kutokana na sababu yoyote zaidi ya iliyoelezwa na Bodi hapo juu,

24. Mtahiniwa yeyote atakayeonekana na hatia ya udanganyifu katika mtihani au kukiuka sheria na kanuni zozote za mtihani atachukuliwa hatua za kinidhamu ambazo zinaweza kupelekea kuondolewa katika ukumbi wa mtihani.

25. Mwisho wa mtihani, vitabu vya majibu vitakusanywa, kuhakikiwa, kufungashwa na kufungwa kwa kushuhudiwa na msimamizi mwandamizi, mratibu wa mtihani wa NBAA na mtahiniwa mmoja wa mtihani.

26. Watahiniwa watafahamishwa matokeo ya mtihani wao mara baada ya Bodi kuwa tayari kufanya hivyo. Matokeo yatawekwa kwenye tovuti ya Bodi na kubandikwa kwenye ubao wa matangazo wa Bodi.