Rasilimali za mafunzo
Maudhui ya Mitaala
Mitaala ya (watunza vitabu vya fedha na wahasibu) imeandaliwa kutoa mwongozo kwa wakufunzi na watahiniwa wanaojiandaa na mitihani ya Bodi itakayopelekea kupata vyeti Watunza vitabu vya fedha (Accounting Technician) na Wahasibu (CPA-T).
Mitaala inaonyesha idadi ya masomo katika kila hatua pamoja na matarajio ya kujifunza kila somo baada kumaliza kipindi cha mafunzo. Mitalaa huonyesha taarifa zitakazoulizwa katika mitihani.
Miongozo ya Masomo
Miongozo ya masomo ni vitabu vya kujifunzia vilivyoandaliwa na Bodi kuendana na mahitaji ya Mitaala. Vitabu hivi vya kujifunzia vinatumiwa na wanafunzi na watoa mafunzo kama njia ya kutoa mwongozo juu ya nini kifundishwe/kujifunza. Miongozo ya masomo inaonyesha maswali ya uzoefu kwa vitendo na mifano halisi kuwasaidia wanafunzi kukumbuka kile walichojifunza. Mwongozo wa masomo hupatiwa kila mwanafunzi aliyejisajili kufanya mitihani ya Bodi. Mwongozo wa Masomo pia unapatikana katika duka la vitabu la Mhasibu (Mhasibu Bookshop) kwa matumizi ya Umma.
Jarida la Mhasibu (The Accountant Journal)
Hili ni jarida la taaluma ya Uhasibu linalochapishwa mara mbili kwa mwaka yaani Januari hadi Juni na Julai hadi Desemba. Jarida hili la Mhasibu linachapisha taarifa zilizofanyiwa utafiti zenye lengo la kuongeza uelewa juu ya maendeleo katika taaluma ya Uhasibu. Jarida la Mhasibu lina uwanda mpana wa wasomaji ambao ni wahasibu, wakaguzi wa hesabu, washauri elekezi wa kodi, wachumi, wakufunzi, watafiti na wanafunzi. Jarida hili linasimamiwa na Bodi ya Mapitio (Editorial Board) inayoundwa na wataalam wafundishaji (Technical resource persons). Mchakato wa uandishi wa Jarida la Mhasibu huongozwa na sera ya Mapitio.
Jamii inashauriwa kuandika machapisho yaliyofanyiwa utafiti katika Jarida la Mhasibu.
Gazeti la Mhasibu (The Accountant Magazine)
Gazeti hili hutolewa mara nne (4) kwa mwaka. Gazeti hili huchapisha maoni na mapendekezo binafsi yanayolenga kujadiliana, kupeana taarifa, ujuzi na uzoefu kwa wataalamu wa wadau wa taaluma ya Uhasibu. Pia, gazeti hili husimama kama chombo cha mawasiliano na matangazo kati ya NBAA, jamii na wadau wake kuhusu maendeleo ya taaluma ya Uhasibu.
Kitabu cha Maswali na Majibu
Kitabu hiki hutolewa na Bodi kwa kila hatua ya Mtihani kwa kila kipindi cha mtihani husika (session). Lengo la kutengeneza Kitabu hiki ni kusaidia wanafunzi kupata mwangaza wa muundo na mtindo wa maswali ya mitihani. Pia Kitabu hiki kinatoa mwongozo wa jinsi ya kujibu mitihani.
Ripoti za wasahihishaji
Ripoti hizi hutolewa na Bodi kila baada ya kusahihisha mitihani. Ripoti hizi huchanganua ufaulu wa wanafunzi katika kila somo, huchanganua maeneo ambayo wanafunzi wapo imara zaidi na maeneo ambayo wapo dhaifu katika kila swali. Ripoti za wasahihishaji zinatoa mapendekezo kwa watahiniwa, watahini, na wakufunzi kwa lengo la kuongeza ufaulu katika mitihani ijayo. Ripoti za wasahihishaji pia zinaonyesha uchambuzi wa ufaulu wa taasisi, nguvu kazi ya Uhasibu inayotengenezwa na Bodi kila mwaka na kwa majumuisho.